Header Ads

ad

Ujue ULAZIMA wa kukata bima kwa chombo cha moto cha usafiri


1. Je, ni kwanini nikate bima?
Jibu rahisi kabisa ni kwamba unakata bima kwakuwa ni jukumu lako kisheria. Sheria ya bima za Vyombo vya Moto (Motor Insurance Act, sura ya 169) kifungu cha 4, inalazimisha chombo chochote kile kuwa na bima kabla ya kutembea barabarani. HIVYO BASI, Kukata bima sio amri ya Polisi bali ni jukumu la kisheria kwa mujibu wa sheria hiyo ya Bunge.

2. Je, ni aina gani ya bima nalazimika kukata?
Sheria inalazimisha mtu mwenye chombo cha moto kukata bima inayojulikana kiingereza kama THIRD PARTY. Aina nyingine zote za bima ni hiyari kuzikata. Kwa ufupi zipo aina nyingi sana za bima ambazo sio lazima kuzikata bali ni hiyari tu. Bima pekee ya lazima ni THIRD PARTY.

3. Kwanini bima ya lazima inaitwa "third party"?
Inaitwa third party kwakuwa bima hii lengo lake ni kumsaidia mtu wa tatu au mtu mwingine Zaidi ya yule mwenye bima mwenyewe. Huyo mtu mwingine anaweza akawa ni abiria uliyempakia, dereva mwenzio uliyemgonga, mtembea kwa miguu uliyemgonga, au mnyama uliyemgonga barabarani au hata miundombinu. 

Ni bima kwaajili ya mtu wa tatu kwakuwa mtu wa kwanza ni Kampuni ya Bima, mtu wa Pili ni Wewe mwenye chombo cha moto na ambaye ndio unakata bima, na mtu wa tatu ni YULE ANAYEDHURIKA KUTOKANA NA MATENDO YA MTU WA PILI, yaani mwenye chombo cha moto au wakala wake. 

Wakala wa mwenye chombo anaweza kuwa dereva wa mwenye chombo, mtoto wa mwenye chombo, au yeyote aliyepewa kuendesha chombo hicho. Hivyo dereva kama chombo si chake, anakuwa wakala wa mwenye chombo.

Katika mkataba huo wa bima Mtu wa kwanza(Kampuni ya bima) na mtu wa pili (Mwenye chombo) huingia mkataba kwa malipo kidogo yaitwayo “Premium”kwaajili ya mtu wa tatu asiyejulikana moja kwa moja. 

4. Kwanini mtu wa kwanza (Kampuni ya Bima) na mtu wa pili (Mwenye chombo) waingie mkataba kwa ajili ya mtu wa tatu?
Watu hawa wawili (first and second party) wanaingia mkataba kwa ajili ya mtu wa tatu, ili ikitokea mtu wa pili kamsababishia madhara mtu wa tatu. Huyo mtu wa Kwanza aweze kubeba gharama au fidia za madhara yaliyosababishwa na mtu wa PILI kwa mtu wa TATU.

5. Kwanini mtu wa tatu akatiwe bima na mwenye chombo (mtu wa pili)
Mtu wa tatu (yeyote aliyepo barabarani) anakatiwa bima na mwenye chombo kwakuwa mwenye chombo ana jukumu la kumlipa fidia  mtu anayemuumiza. 

Yaani wewe Juma(dereva bodaboda) ukinipakiza kwenye bodaboda yako ikatokea umenidodosha na mie kuumia basi ujue una wajibu wa kunilipa fidia kwa maumivu uliyonisababishia. Au ikitokea wewe Juma umegonga chombo changu cha moto au umemgonga mwanangu, basi ujue una wajibika kunilipa.

IKIWA utakuwa na bima ya third party gharama za matengenzo ya bodaboda uliyoigonga, matibabu ya uliowagonga nk vyote vitabebwa na kampuni ya bima. Wewe jukumu lako litakiuwa ni kutoa taarifa tu kwa kampuni ya bima kuwa umesababisha ajali. Lakini kama utakuwa hauna bima ya third party ina maana gharama hizi zote utazibeba wewe mwenyewe.

6. Kwanini serikali imeweka ulazima wa kukata boma?
Serikali imeweka ulazima wa kuwa na hiyo bima kwenye vyombo vya moto ili kuwakinga wananchi wake wanaoumzwa na wenye vyombo vya moto. Pia ni sehemu ya kuwawajibisha wenye vyombo vya moto kubeba gharama za madhara waliyoyasababisha. Mwenye chombo cha moto asingepewa jukumu hili, serikali ingekuwa inaingia gharama kubwa sana kugharamia madhara yaliyosababishwa na wewe dereva au mmiliki wako.

7. Je, bima ya third party, inakukinga wewe na chombo chako?
Kama tulivyokwisha kuona hapo juu, jibu ni HAPANA. Bima ya third party hailipi gharama za madhara ya kuharibika chombo chako au wewe mwenyewe kuumia, bali inalipa gharama za madhara ya kuharibika chombo cha mtu mwingine au mali ya mtu mwingine kuharibika.

8. Je, bima ipi itanikinga mimi na chombo changu?
Ili usaidike wewe na chombo chako unatakiwa kukata BIMA MSETO (COMPREHENSIVE) au wengine huita BIMA KUBWA. Bima hii kubwa faida yake ni kwamba kukitokea ajali wewe ukauma, chombo chako kikaharibika na pia mali ya mtu mwingine ikaharibika na mtu mwingine kuumia, basi wote nyie gharama  zitabebwa na bima hii. Bima hii bei yake ni kubwa kidogo kuliko ile ya third party. Na bima hii sio ya lazima.

9. Hitimisho
Kwa hiyo bima ya third party sio kwaajili yakow ewe na chombo chako, bali ni kwaajili ya watu wengine na mali zao, ambazo wewe unaweza kuziharibibu au kuwaumiza kutokana na udereva wako. Kwa ufupi ndio kusema kwamba ikiwa umepata ajali kwa kumgonga mtu mwingine na chombo chako kimeumia, basi ile bima yako ya third party itamlipa yule aliyeumia, lakini wewe haitakulipa. 

Gharama za kujitibia wewe binafsi na matengenezo ya chombo chako utajigharamia wewe mwenyewe. Ila kama una bima kubwa, basi itakugharamia na wewe.

NATUMAI HADI HAPO UTAKUWA UMEPATA MWANGA KUHUSU BIMA HUSUSAN BIMA YA THIRD PARTY

No comments