Header Ads

ad

EQUIP wawezesha kiwango cha elimu Tabora kuimarika

Picha ya maktaba, ikiwaonyesha wanafunzi wa madarasa mawili wakiwa kwenye darasa moja. Ni mazingira magumu ya kusomea kama haya, ambayo Equip wamekuwa wakijitahidi kuyafanyia kazi katika mikoa 9 nchini, ukiwemo wa Tabora.

MRADI wa EQUIP unaojishughulisha na uboreshaji elimu katika mikoa tisa hapa nchini umepongezwa kwa dhamiria yake ya dhati ya kuboresha kiwango cha elimu katika mkoa wa Tabora ikiwemo kumaliza tatizo la utoro sugu mashuleni.

Hayo yamebainishwa na Afisa Elimu wa Mkoa huo Suzan Nusu alipokuwa akifungua na kuchangia mada katika semina ya siku mbili ya wandishi wa habari wa mkoa huo iliyoandaliwa na Mradi wa Kuboresha ElimuTanzania (EQUIP).

Alisema tangu mradi huo uanze kazi mkoani hapa mafanikio yameanza kuonekana kwa mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa 10 bora huku baadhi ya shule zake zikishika nafasi za juu kitaifa.

Aidha takwimu za sasa zinaonesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la kiwango cha ufaulu ikiwemo kupungua kwa vitendo vya utoro na mimba mashuleni.

‘Mradi wa EQUIP umetusaidia sana kwani usimamizi wa shule umeboreshwa kwa kiasi kikubwa na walimu wamepewa mafunzo ya kutosha katika suala zima la kuboresha mbinu za ufundishaji darasani’, alisema.

Aliwataka wana habari kusaidia kutangaza mpango huo katika vyombo vya habari ili wananchi wauelewe na waweze kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha jitihada hizo.

Suzan alifafanua kuwa kwa muda mrefu mkoa huo ulikuwa haufanyi vizuri katika matokeo ya darasa la saba na sekondari lakini baada ya kuletewa mradi huo hali imebadilika sana kwani mkoa huo sasa ni miongoni mwa mikoa 10 bora hapa nchini tofati na awali.

Alipongeza jitihada nzuri zinazofanywa na mradi huo ikiwemo kuanzishwa klabu ya wanafunzi ya ‘Jiamini Uwezo Unao-JUU ),  kutoa usafiri wa pikipiki kwa Maafisa Elimu kata wote na kuhamasisha uanzishwaji shule za utayari kwa watoto wadogo katika vitongoji na vijiji vyote vilivyoko mbali na maeneo ya shule.

Kiongozi wa Mradi huo Mkoani hapa Dk Mary Soko alitaja mafanikio yaliyopatikana kupitia mpango huo kuwa ni kuanzishwa kwa Mafunzo kazini  (INSET Training), Ushirikiano baina ya wazazi na walimu (PTP) katika kila shule na kuongeza usimamizi na mwamko wa elimu kwa wazazi na watoto wao.

Aidha alisema serikali kwa kushirikiana na EQUIP wameweza kuboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya shule katika halmashauri zote za mkoa huo ikiwemo kutoa mafunzo ya weledi kwa walimu wa shule hizo.

Alitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuunga mkono jitihada hizo na zile zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano ili kuboresha suala zima la elimu hapa nchini ikiwemo kuhakikisha watoto wote wanasoma shule.

Akitoa mada katika semina hiyo Afisa Mawasiliano wa EQUIP kutoka DSM Mwanaidi Msangi alisema hadi sasa wamegawa jumla ya pikipiki 200 kwa Maafisa Elimu Kata wote wa mkoa huo ili kuboresha utendaji wao katika suala la elimu.

Aidha alisema kupitia program hiyo walimu zaidi ya 36,000 wa shule za msingi wakiwemo walimu wakuu wamepewa mafunzo maalumu ili kuboresha taaluma zao na kuwaongezea weledi na mbinu za ufundishaji darasani katika mikoa hiyo.

Afisa Mafunzo wa EQUIP mkoani hapa Sofia Nyanda alisema mradi huo unatekelezwa katika mikoa 9 hapa nchini ikiwemo mkoa wa Tabora, mikoa mingine ni Mara, Simiyu, Shinyanga, Katavi, Singida, Dodoma, Lindi, na Kigoma.

No comments