Header Ads

ad

Wenger azidi kumficha Antonio Conte ... Arsenal yaigaragaza Chelsea na kutwaa Ngao ya Jamii

Arsene Wenger, na wachezaji wake wakifurahia kuibwaga Chelsea na kutwaa Ngao ya Jamii

Klabu ya soka ya Arsenal, imezindua msimu mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza, kwa kuendeleza ubabe wake wa siku za hivi karibuni dhidi ya Chelsea, ubabe ambao umeanza kujidhihirisha tangu miamba hao wa Darajani, waanze kufundishwa na muitaliano Antonio Conte. 

Katika pambano la wikiendi hii, la kuwania ngao ya jamii, pambano ambalo kwa kawaida ndio kiashiria cha kuanza msimu mpya wa EPL, Arsenal, waliweza kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 5-2, katika mechi hiyo ambayo mshindi alipatikana kupitia njia ya penalti, baada ya mechi kumalizika dakika 90, huku timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1. 

Arsenal, walilianza pambano hilo kwa kutawala mchezo na kusababisha purukushani za hapa na pale langoni mwa Chelsea, lakini wakashindwa kutumia utawala huo kujipatia bao la kuongoza, ambapo Chelsea hatimaye waliweza kutulia nao na kuanza kusukuma mashambulizi ya kushtukiza langoni mwa Arsenal. 

Hata hivyo, timu hizo hazikuweza kutambiana hadi nusu ya kwanza ya mchezo inamalizika. 

Chelsea walikianza kipindi cha pili kwa kujiandikishia bao la kuongoza mapema tu katika dakika ya pili ya kipindi cha pili, kupitia kwa Victor Moses, ambaye alifunga kutokana na uzembe wa mabeki wa Arsenal. 

Timu zote ziliendelea kushambuliana kwa kushtukizana, ambapo hadi kufikia dakika ya 78, ilionekana kama Chelsea walikuwa wanaelekea kuwa washindi wa mechi hiyo, kwani sio tu kuwa walikuwa wametawala pambano na kujenga mashambulizi ya hapa na pale, bali pia walikuwa wakililinda vyema bao walilokuwa wamejipatia. 

Hata hivyo, kama wahenga walivyosema kuwa mpira ni mchezo wa dakika 90, na kwamba kabla ya filimbi ya mwisho, usiseme kuwa haiwezekani, ndivyo ambavyo Arsenal walifanya kwa kujipatia bao la kusawazisha lililowekwa kimiani na Sead Kolasinac , ambaye aliunganisha kimiani vyema mpira wa adhabu uliokuwa umepigwa na Granit Xhaka. 

Adhabu hiyo, ilitolewa baada ya Pedro kumxhezea madhambi Mohamed Elneny, kosa ambalo pia lilimfanya azawadiwe kadi nyekundu na mwamuzi. 

Baada ya hapo, timu zote zikaamua kufunguka, na ikawa shughuli ya mbele kwa mbele kila upande, huku Chelsea wakiwa pungufu. Hata hivyo, haikuweza kupatikana mbabe kati yao, hadi dakika 90 zinakatika. 

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano za EPL, pambano la Ngao ya Jamii, huamuliwa kwa njia ya matuta, ikiwa timu zinamaliza dakila 90 zikiwa sare. Hivyo basi, timu zikapigiana penalti, ambapo Arsenal walipata penalti 4, huku Chelsea wakipoteza mbili na hivyo kuwaachia Arsenal ushindi huo. 

Ushindi huu, umekuja ikiwa ni chini ya miezi mitatu, tangu Arsenal wawachape Chelsea katika fainali ya kombe la FA, mwishoni mwa msimu uliopita, katika uwanja huo huo wa Wembley. 

Aidha, ni ushindi wa tatu kati ya mapambano manne rasmi zilizowakutanisha Wenger na Conte. 


No comments